Saturday, July 11, 2015

CV YA MAGUFULI HAPA SOMA.

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza
rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake
wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa
ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza
rasmi azma yake.
Dk. Magufuli, amekuwa mbunge tangu mwaka
1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo,
alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Wizara
iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah.
Anajulikana kama kipenzi cha aliyekuwa Rais wa
Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa, ambaye mara
kadhaa hakusita kumsifu hadharani, akimtaja
kama mmoja wa ‘askari wa miavuli’ katika baraza
lake la mawaziri.
Aidha, uhusiano wake na Mkapa umejidhihirisha
hadi kwenye masuala ya kifamilia, ambako mara
kadhaa rais huyo mstaafu ameweza kuhudhuria
hafla na misiba mbalimbali nyumbani kwa Dk.
Magufuli.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk.
Magufuli alipewa fursa kwenye Mkutano Mkuu wa
CCM kusoma mafanikio ya chama hicho kwenye
utekelezaji wa ilani yake upande wa barabara.
Uwezo wake wa kukariri takwimu mbalimbali,
ulikuwa kivutio kwenye mkutano huo na sehemu
nyingine kama bungeni ambako hutakiwa kueleza
mafanikio ya wizara yake.
Hivi karibuni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Ali
Hassan Mwinyi, alimsifu kwa kumtaja kama
‘simba wa kazi’ kutokana na uchapaji kazi wake
katika wizara mbalimbali ambazo ameziongoza.
Kwa upande wa wananchi, wengi wanamuona Dk.
Magufuli kama mmoja wa mawaziri wachapakazi
waliowahi kutokea katika historia ya taifa hili.
Hata hivyo, waziri huyo amekuwa akikosolewa
kwa uamuzi wake wa uuzaji nyumba za Serikali
kwa watumishi na hata wasio watumishi wa
umma.
Pamoja na dosari hiyo, watetezi wake wanaamini
kilichofanywa wakati huo wa utawala wa awamu
ya tatu kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Baraza
la Mawaziri, na si uamuzi wa Dk. Magufuli
mwenyewe.
CV yake
Dk. John Pombe Joseph Magufuli, alizaliwa
Oktoba 29, 1959 wilayani Chato – wakati huo
ikiwa Mkoa wa Kagera (sasa Mkoa wa Geita).
Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009)
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 1991 – 1994, alisoma Shahada ya Uzamili
(Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na
baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza.
Mwaka 1985 – 1988, alisoma Shahada ya Kwanza
ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1981 – 1982, alisoma diploma katika
Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia
na Hisabati.
Mwaka 1979 – 1981, alipata elimu ya juu ya
sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa,
Iringa.
Mwaka 1977 – 1978, alisoma elimu ya sekondari
katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.
Mwaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi
Katoke, Biharamulo mkoani Kagera.
Mwaka 1967 – 1974, alisoma Shule ya Msingi,
Chato.
Mafunzo
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani
Dodoma.
Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT
Makuyuni, Arusha.
Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT
Makutupora, Dodoma.
Uzoefu wa kazi
Mwaka 2010 – hadi sasa: Waziri wa Ujenzi na
Mbunge wa Chato.
Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo
Mashariki (Chato).
Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo
Mashariki (Chato)
Mwaka 2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi, na
Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi; na
Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika
cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), Mwanza.
Mwaka 1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari
Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na
Hisabati).
Dk. Magufuli amepata tuzo mbalimbali za ndani
na nje ya nchi.
Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa
na kimataifa.
Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa
na ana watoto kadhaa.

No comments:

Post a Comment