Saturday, July 11, 2015

Mbinu za kurejesha penzi lililokufa?

UNATAKA KUREJESHA PENZI LILILOKUFA ?
by roryamaendeleo
20 minutes ago
ASALAMALEIKUM ndugu zangu Waislamu ambao mpo
ndani ya mfungu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan . Bila
shaka shaka swaumu inapanda na ishallah Mungu
atawafanyia wepesi mtaumaliza mwezi huu salama .
Nikirudi katika mada yangu ya leo, nazungumza zaidi na
wale ambao walikuwa wapenzi lakini kutokana na
sababu mbalimbali walifikia hatua ya kutofautiana . Penzi
lao likaota mbawa .
Wameona sera zao haziendani , wakaamua kuachana .
Kila mmoja anaanza kutafuta pumziko lingine kwa muda
wake .
Lakini wakati hayo yakiendelea , kuna mmoja kati ya
wawili hao anakuwa ameguswa na ugomvi wao .
Anataka kurejesha penzi , hajui ataanzia wapi. Huyo ndiye
ninayezungumza naye leo hapa.
Vipo vitu vya msingi vya kutafakari kabla hujaamua
kufufua penzi lililokufa , ni vyema ukajifunza :
JITATHMINI
Kabla hujaamua kufufua penzi lililokufa kwanza
unapaswa kujitathmini juu ya penzi lako la awali na
sababu ya kuachana kwenu . Jiulize ni nini kilisababisha
hadi mkafikia hatua ya kuachana ?
Pima uzito wa sababu hizo za kuachana kabla ya kuamua
kuomba nafasi upya . Sababu hiyo inaweza kubadilika au
haiwezekani ? Usije ukawa sababu ya kuachana kwenu ni
mwenzako kukwambia anaolewa na mtu mwingine
halafu wewe ukaendelea kulazimisha kuomba nafasi.
Sababu ya kuachana kwenu ikiwa ni ya yeye kupata
bwana wa kumuoa na mipango tayari imeshafika
patamu, huna haja ya kuendelea kurejesha penzi hilo
maana tayari linakuwa limeshafika hatua ambayo huwezi
kulizuia .
Jiulize nani alikuwa chanzo cha mgogoro ? Chanzo chake
ni nini ? Ukishagundua chanzo chake na nani alikuwa
anasababisha, anza kutafuta suluhu kwanza moyoni
mwako .
Jitathmini kama chanzo kilikuwa ni tabia yako wewe
labda mfano hasira , jiulize unaweza kubadilika ? Ufanyeje
ili uweze kubadilika ? Ukishabadilika, hauwezi kurudia
tena tabia hiyo?
Hakikisha kwanza unajishughulikia matatizo yako . Katika
maeneo yote ambayo wewe ulihusika, hakikisha
unajisahihisha mwenyewe ndipo baadaye utamshirikisha
mwenzako pindi utakapokuwa umekutana naye kwa ajili
ya mazungumzo.
TAZAMA VIKWAZO
Wakati unatafuta muda wa kukutana na mwenzi wako ,
jiulize kwa wakati huo ana kikwazo gani ? Yawezekana
wakati mnaachana hakuwa na kikwazo lakini wakati
unataka kurejesha penzi , unakuta mwenzako ana
kikwazo.
Hawezi kurudiana na wewe wakati huo tayari yupo katika
mikakati ya kufunga ndoa na mtu. Au yupo na mtu
ambaye tayari wameendana , wameshatambulishana kwa
wazazi na kuweka mikakati ya ndoa .
ANDAA SULUHU
Ukishabaini chanzo , sababu na kujiridhisha kwamba
umeshafanyia kazi upungufu wako , omba nafasi ya
kukutana na mwenzi wako. Ikiwezekana watumie hata
watu wake wa karibu ili wakusaidie kukukutanisha naye .
Muombe radhi. Mueleze kwamba umeshayafanyia kazi
matatizo yako . Umebaini tatizo na uko tayari kwa suluhu.
Hata katika maeneo ambayo yeye alikuwa akikosea,
tumia lugha nzuri kumueleza namna ambavyo anapaswa
na yeye kubadilika ili msijikute mnaingia tena kwenye
migogoro.
Usimlamu. Onesha dhamira ya dhati ya kutaka kuishi
kama zamani . Mpe nafasi pia akueleze vitu ambavyo
pengine ulikuwa unamkwaza . Vikubali na ahidi kuvifanyia
kazi .
Akikuelewa , ongeza upendo maradufu. Ishi kwa
kujikumbusha kila siku maeneo ambayo ulikuwa
unayakosea . Usirudie makosa . Hakika mtaheshimiana na
mtafurahia penzi lenu na kila mmoja akihofia kumuudhi
mwenzake .
Mara nyingi penzi lililokufa likifufuka huwa linakuwa
tamu , linakuwa na matokeo mazuri zaidi ya lile la awali .
Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa , tukutane
wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri .

No comments:

Post a Comment